Sportstain kama wadau wa habari tutakuwa miongoni mwa watu hao wenye nia thabiti ya kuleta mapinduzi ya mpira wa miguu nchini kote, kuanzia mashindano ya mashuleni kwa ngazi zote, mitaani, ligi zote za madaraja ya chini n.k.
Rais Karia umetwaa kiti hiki kikuu cha TFF wakati huu ambao hatuwezi kusema kuwa umelikuta soka likiwa na hali mbaya sana na wala haliko katika hali nzuri kimaendeleo ikilinganishwa na nchi nyingine barani Afrika ambazo kwa kiasi fulani zimepiga hatua (mfano hasa ni nchi za Magharibi na Kaskazini mwa Afrika na sasa nchi ya Afrika Kusini kwa mzee wetu Madiba "R.I.P")
Bado hujachelewa ukiwa kama mkuu wa TFF unayo nafasi kubwa ya kuleta madiliko makubwa kwenye soka letu ambalo kwa kiasi kikubwa macho ya walio wengi yameelekezwa kwenye ligi kuu ya Vodacom (VPL) hasa timu mbili ama tatu tu na nyingingine zikibaki kuwa washiriki tu na si washindani wa ligi hiyo huku zikigubikwa na lindi kubwa la ukata wa pesa.
Isotoshe wewe unaweza kuwa rais wa shirikisho mwenye bahati kwakuwa umekuja wakati ambao teknolojia ya mawasiliano duniani imetamalaki kwahiyo unayo nafasi ya kuweza kujipatia habari kutoka kila kona ya dunia na kujifunza pia kutoka kwa wenzetu ambao ambao tayari wameshafika mbali na sasa wanautumia mchezo huu kama sehemu ya biashara kubwa na si sehemu ya kujenga urafiki na kuimarisha afya zetu kama tulivyofundishwa mashuleni.
![]() |
| Bwana Wallace Karia, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) 2017-2021. |
Yawezekana kila mdau wa mchezo huu akawa na kosa kwa nafasi yake lakini hatutakuwa watu wa maana kama tutautumia wakati huu kuwa wa kutafuta mchawi ni nani, bali inatakiwa nguvu kubwa na maarifa vielekezwe kwenye kutafuta suluhu na kuleta maendeleo ya mpira wa miguu nchi nzima kwa kushirikiana vyema na wadau mbalimbali ikiwemo serikari, mashirika, makampuni, taasisi, vyombo vya habari na hata mtu mmoja mmoja.
Mheshimiwa rais Karia, ifike wakati sasa Tanzania ijivunie kuwa na wachezaji walau wawili watatu wa hadhi ya Samatta kabla hujamaliza muhula wako wa kwanza madarakani kwasababu watoto wenye vipaji wapo wengi tu lakini misingi ndicho kitu pekee kinachokosekana.
Na hata wazazi wa watoto majumbani wanatakiwa waondolewe hofu kuu juu ya watoto wao wanaocheza mpira kwamba wanaweza kuumia hatimaye wapate vilema vya kudumu ama la watashindwa kufanya vizuri kwenye masomo yao.
Na mbaya zaidi imejengeka dhana miongoni mwa jamii kwamba wanaocheza mpira ni wale walioshindwa elimu, dhana hii imeua vipaji vingi sana miaka nenda rudi.
Ni wakati wako wa kushirikiana na wataalam wa biashara na makampuni ya bima nchini ili nayo yaanze kuwekeza kwenye mashindano ya watoto mashuleni na mitaani ili kuondoa hofu ya wazazi kugharamia matibabu ya watoto wao pindi waumiapo viwanjani, zitengenezwe sera na utaratibu mzuri ili makampuni haya ya bima yaweze kuingia kwa miguu yote miwili.
Bahati kuu iliyoje kwako kwa kuwa rais wa shirikisho hili ambalo watu wengi ndani yake ni wapenzi wa soka ukilinganisha na nchi nyingine kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki, hili wala halihitaji uwe umebobea kwenye elimu ya utafiti bali linathbitika dhahiri.
Sportstain kama wadau wa habari tupo hapa na tutatoa ushirikiano kwa shirikisho lako na kwa kila mdau wa sekta hii ya michezo ili kukuza na kuendeleza michezo nchi nzima.
Tunakutakia kazi njema
(Mwandishi wa makala hii ni Davis Mwakalosi usisite kuwasiliana nami kwa email yetu ya sportstz17@gmail.com kwa habari, maoni, ushauri na hata ukitaka kukosoa unakaribishwa pia.)

Good history, hakika Huyu ni Jembe
ReplyDeleteAnaonekana ni mtu wa mipango thabiti, Mungu amjalie afya na ushirikiano mzuri na wote wanaomzunguka soka litafika pazuri someday
Delete